Sunday, January 18, 2015

JINSI YA KUUTAMBUA WITO ULIOITIWA


Na: ERASTO KIBIKI


Katika biblia neno “wito” lina maana kubwa sawa na maana yake katika lugha ya kila siku.  Maana hiyo pia inahusika kama biblia inasema habari za wito wa Mungu kwa watu binafsi, ingawa maana nyingine zina alama nyingine za matumizi ya mafundisho ya kidini.
Mungu anaita watu katika maana ya kuwaamuru au kuwakaribisha, kama Isaya anavyoelezea jinsi Mungu alivyoita na watu hawakuitika alivyonena na watu hawakusikiliza; anasema “Mimi nitawaandikia kuuawa kwa upanga na ninyi nyote mtainama ili kuuawa kwa kuchinjwa, kwa sababu NILIPOITA HAMKUITIKA, NILIPONENA HAMKUSIKIA; bali mlitenda yaliyo mabaya machoni pangu, mlichagua mambo nisiyoyafurahia” [Isaya 65:12].

Hapa tunaona hawa watu walifanya uchaguzi binafsi na kuukataa wito wa Bwana juu ya maisha yao, kisha wakachagua mambo yasiyomfurahisha Mungu na wakaishia kuuawa na kuchinjwa. Ndivyo ilivyo na kwetu hata sasa, mara nyingi wito halisi una upinzani mkubwa sana. Kupandishwa cheo kazini au kupata kazi Fulani inaweza ikawa ni kuanguka kwako katika wito ulioitiwa na kukusababisha uzichague njia zako mwenyewe na si njia za Bwana.

Pia Yeremia anaandika kuwa “Na sasa kwa sababu mmezifanya kazi hizi zote asema BWANA, nami nikasema nanyi, nikiamka mapema na kunena, lakini hamkusikia; NAMI NIKAWAITA WALA HAMKUITIKIA” [Yeremia 7:13]

Hawa watu wamezifanya kazi zao wenyewe, yaani wametimiza kusudi la kuishi kwao duniani bila ya Mungu kuhusika, wamefanya yote kwa matakwa yao wenyewe,kisha Mungu akasema nao, akiamka mapema sana na kunena habari za WITO WALIOITIWA na kusudi la kuishi kwao duniani, na ya kuwa wageuke na kuziacha njia zao mbaya na kumuelekea Mungu wao milele lakini HAWAKUSIKIA, na walipoitwa HAWAKUITIKA.

Mungu anakuita hata sasa, anataka urudi kwenye asili yako, uenende kama ulivyoitwa, wewe umeitwa uwafundishe watu KWELI ya Neno la Mungu, badala ya kwenda ulikoitwa, umejikuta ukiwa BANK Teller au Mhasibu na kufungiwa kwenye kachumba ukihesabu pesa wakati mamilioni ya watu wanaelekea JEHANAMU kwa kukataa kuishi kama ulivyoitwa.

“… Mwenende kama inavyoustahili WITO WENU MLIOITIWA, kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo, na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho, katika kifungo cha Amani” [Efeso 4:1-3]
Zaidi ya hayo Mungu ANAWAITA watu katika maana ya KUWATEUA na KUWAONGOZA kwa kadiri ya makusudi yake maalumu.

Isaya 43:1 inasema “Lakini sasa, BWANA aliyekuhuruku, Ee yakobo, Yeye aliyekuumba Ee Israeli asema hivi; Usiogope maana nimekukomboa; NIMEKUITA KWA JINA LAKO, wewe u wangu” hapa tunaona Mungu akiwaita watu na kuwateua wawe wake, anawaongoza na kuwapa mwelekeo maalumu wa maisha.
Ukijua kuwa duniani tu wapitaji na wasafiri tusiokuwa na makao ya kudumu, utajua kuwa haikupasi kuishi vile unavyotaka wewe bali unapaswa kutenga muda na kulitafuta kusudi la kuishi kwako na hapo ndipo utakapoenda kama wito wako ulivyoitiwa.

Isaya 46:11 inasema “Nikiita ndege mkali kutoka mashariki, mtu wa shauri langu toka nchi iliyombali; Naam, NIMENENA, NAMI NITATEKELEZA; NIMEKUSUDIA, NAMI NITAFANYA” asema Bwana wa Majeshi.

Mungu amekuitia kusudi maalumu la kuishi kwako naye amenena kuwa ATATEKELEZA,  na amekusudia kukuita hivyo ATAFANYA lile alilokuitia. Hautatembea peke yako katika huo wito na hilo kusudi uliloitwa; Mungu yupo nawe, songa mbele utafika.

Hosea 11:1 anaelezea kuwa “Israeli alipokuwa mtoto, naalikuwa nikimpenda, NIKAMWITA mwanangu atoke Misri” hapa Mungu alimpenda Israeli tangu utoto wake na AKAMWITA ili aliishi kusudi la KUITWA kwake. Lakini mstari wa pili wa hii hosea 11 unasema hivi “kadiri WALIVYOWAITA ndivyo walivyoondoka na kuwaacha; waliwatolea dhabihu mabaali na kuzifukizia uvumba sanamu za kuchonga”

Kumbe unaweza ukawa unaukataa wito wa Mungu maishani kwa sababu kuna watu au vitu vya kidunia vikikuita na kuuchukua muda wako wote na hatimaye maisha yako, kuna watu wameitwa na kuvutwa na MISHAHARA, PESA, BIASHARA, NDOA, KAZI n.k

Ni nini kilichokufanya uukatae WITO ulioitwa? Hicho ndicho kilichokuita, nawe umekifuata na kukiabudu. Ndio maana unashindwa kurudi kwenye kusudi la maisha yako.

“Kwa Imani Ibrahimu ALIPOITWA aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi, akatoka asijue aendako” [Ebrania11:8]

Kukubali kutoka hapo ulipo na kwenda mahali unapoambiwa uende na wewe hupajui kisha ukaanza safari ya kwenda, hapo ndipo tunaposema UMEITIKA NA UMEUKUBALI WITO WAKO. Wengine wameitwa wakae Madhabahuni lakini wao wapo maofisini, wengine wameitwa kwenye biashara na kwenye uongozi lakini wapo madhabahuni. Hii inaonyesha kuwa KUUJUA  WITO ulioitwa unapaswa kuwa na utulivu wa kina mbele za Mungu.

Mtume Paulo anaelezea uhakika wa kuitwa kwake kwenda Makedonia kuihubiri injili akisema “Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa TULIONA HAKIKA ya kwamba MUNGU AMETUITA tuwahubiri habari njema” [Matendo 16:10]. Uhakika huu ulitokana na maono ya Mungu kwao, nasi imetupasa kukaa magotini pa Mungu aliyehai na kwenda katika njia zake milele.

Katika maana ya juu zaidi, Mungu anapowaita watu mbalimbali katika kazi yake huwa ANAWAITA kwa kuwapa WOKOVU wake na kuwafanya wawe wake kabisa.
Wakristo ni watu walioitikia WITO wa Mangu katika injili …..

Itaendelea………………………….


No comments:

Post a Comment