Wednesday, October 1, 2014

UMUHIMU WA TOBA KWA KANISA LA SASA

Mwl. Elia Agrey
SEHEMU YA PILI

Baada ya kuangalia maana ya TOBA katika ile sehemu ya kwanza kama ambavyo tuliona kuwa TOBA ni kugeuka kutoka katika jambo ambalo Mungu amelikataza na kutenda lile ambalo Mungu ameliagiza kufanya au kutenda.

Katika sura hii nataka tuangalie UMUHIMU wa TOBA kwa kanisa la sasa ambalo ni mimi na wewe uliyepata nafasi ya kusoma somo hili

1.    TOBA INAKUSOGEZA KARIBU NA MUNGU ZAIDI

Toba ya kweli inakusogeza karibu na Mungu na kuyarudisha mahusiano kati ya mtu na Mungu ambayo yaliharibiwa na dhambi.Ule uadui ambao dhambi iliuweka kati yako na Mungu unaondolewa na Mungu anakuwa rafiki yako wa karibu.

“…Warumi 3:23 kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;..”

Dhambi inafanya Utukufu wa Mungu upungue katika maisha yako na namna ambavyo Mungu anajidhihirisha kwako kuwa katika kiwango cha chini.Unaposoma huu mstari unagundua na kujifunza kuwa kama Dhambi inafanya UTUKUFU wa Mungu kwako kupungua basi TOBA inafanya UTUKUFU wa Mungu kwako kuongezeka zaidi na zaidi, kwa hiyo unapotubu unamfanya Mungu azidi kujifunua na kujidhihirisha zaidi katika maisha yako. 

Dhambi ambazo zinafanywa na kanisa la Mungu linamfanya Mungu apunguze udhihirisho wake katika kanisa na vivyo hivyo dhambi zinazofanywa na Nchi au taifa zinafanya Mungu apunguze udhihirisho wake katika Taifa. Toba kwa ajili ya Kanisa inamfanya Mungu aongeze udhihirisho wake katika kanisa lake na Toba kwa ajili ya Nchi inamfanya Mungu aongeze zaid udhihirisho wake katika nchi.

Angalia kitabu kile cha “…Isaya 57:15 Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu…”

Sio kila mtu anakaa pamoja na Bwana ingawa wengi wanapenda kukaa pamoja na Bwana lakini ni wale walio na roho iliyotubu ndio wanaopata nafasi na fulsa ya kukaa pamoja na Bwana.

Unapotubu kwa roho na kweli Mungu anasema anakusogeza karibu naye na kukaa pamoja na wewe siku zote.Kwa iyo kanisa linapokuwa na roho ya toba ndipo Mungu anakaa katikaki yake na ndipo UWEPO wa Mungu unalifunika kanisa na kulitawala mahali kote na kwa sababu Mungu anakaa milele basi kwa kupitia TOBA kanisa linakaa pamoja na Mungu milele.

Ukielewa umuhimu wa TOBA unapokuwa umemkosea Mungu wewe kama kanisa la Mungu hautakaa katika hali ya kuto tubu bali utazitubia dhambi zako zote maana kwa kupitia TOBA Mungu anakusogeza karibu naye zaidi na zaidi.

Unaposoma katika Biblia unaona watumishi wa Mungu mbali mbali wakikosea kwa namna moja ama nyingine lakini walipochukua uamuzi wa kurudi kwa Mungu na kuomba msamaha tunaona Mungu akiwasamehe na kuwasogeza karibu zaidi na UWEPO wake. Kwa hiyo hata na kwako wewe ni muhimu ukajifunza namna ya kurudi kwa Mungu kwa njia ya TOBA na ndipo Mungu atakusogeza karibu zaidi na UWEPO wake.

Damu ya YESU KRISTO ipo ili ikusamehe na kukusafisha zaidi na kukufanya uwe safi haijalisha ukubwa wa kosa au udogo wa kosa unapo TUBU Mungu anakusamehe na kukufanya kuwa safi kisha kukusogeza karibu naye.

Hakuna kosa ambalo ni kubwa sana kiasi cha kutosamehewa na Mungu,Mungu ni Mungu wa msamaha unapotubu na Damu ya YESU ipo kwa ajili ya makosa ya watu ili kuwasamehe na kuwatakasa kila siku iitwapo leo ili kuwaleta watu walio safi pasipo na taka yoyote ndani yao mbele za Mungu aliye Mtakatifu.

1 Petro 2:9-10 “…Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema…”

Unaposoma huu mstari unaona Petro anajaribu kuwaonyesha hawa waliotubu dhambi zao na kumwamini Bwana Yesu katika maisha yao kitu kilichotokea baada ya wao KUTUBU na kumwamini Kristo anasema ninyi ni mzao mteule maana yake ni kuwa ninyi sasa ni uzao wa Mungu uliotokana na Mungu mwenyewe na ni familia ya Mungu mwenyewe na ni watu walio karibu na Mungu na wanaoishi na kukaa mahali ambapo Mungu yupo.

hivyo unapotubu dhambi zako na kurudi kwa Mungu wewe unakuwa sio mtu wa kawaida bali mtu wa tofauti unae kaa mahali ambapo Mungu anakaa. Kwa hiyo tunapotubu kama Kanisa la Mungu,Mungu Baba anazidi kutusogeza karibu na yeye zaidi nasi tunapata kumjua Mungu zaidi na TABIA ya Mungu inakuwa TABIA ya KANISA na vitu avipendavyo Mungu ndivyo nasi kama KANISA tunaanza kuvipenda

Uhusiano uliopotea kati yako na Mungu unarudi kwa njia ya TOBA pekee.

2. TOBA INAWEKA ULINZI KATIKA MAISHA YAKO

Jambo la pili ambalo TOBA inafanya katika maisha ya mtu anae TUBU ni kuweka ulinzi katika maisha yake.
Ayubu 1:5-10 “…5 Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote.
 6 Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao.
 7 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.
 8 Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.
 9 Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure?
 10 Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi…”

Bwana Yesu apewe sifa!!! Unaposoma katika hii mistari unaona jinsi ambavyo Mungu na shetani wakizungumza juu ya mtumishi wa Mungu Ayubu.Shetani alikuwa katika kuzunguka zunguka huku na huko humo ndipo akakutana na Mungu na Mungu anamuuliza shetani kama amekutana na mtumishi wake Ayubu

Mstari ule wa tisa na kumi anasema “… Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi…”

Mungu hakuanza tu kumzingira Ayubu pande zote bila sababu pasipo Ayubu kufanya kitu chochote,Ayubu alikuwa na utaratibu wa kuomba TOBA kwa Mungu kwa ajili yake na kwa ajili ya familia yake,mke wake na watoto wake na alipokuwa akiomba TOBA kwa ajili yake na familia yake NDIPO Mungu alijenga UKIGO au UKUTA au WIGO kuwazunguka pande zote kiasi ambacho shetani hakuona sehemu ya kuingilia kwa Ayubu na kwa familia yake yote aliyokua anaiombea TOBA kwa Mungu hata pasipo familia yake kujua kuwa inaombewa TOBA.

Jambo la msingi kuelewa ni kuwa unapoomba TOBA ya kweli kwa Mungu, Mungu anaachilia ulinzi katika maisha yako, hauhitaji kuomba ulinzi unahitaji kuomba TOBA na Mungu ana kusamhehe na kuachilia ulinzi wake katika maisha yako.

Adui hawezi kuyagusa maisha yako tena maana Mungu anakulinda pande zote, kukugusa kwake ni pale ambapo Mungu ameuondoa WIGO wake kwako kwa kusudi maalumu na kumruhusu shetani akujaribu.



No comments:

Post a Comment