Wednesday, September 24, 2014

UMUHIMU WA TOBA KWA KANISA LA SASA

SEHEMU YA KWANZA

Mwl: Elia Agrey

MAANA YA TOBA

Bwana YESU apewe sifa; ninayo kila sababu ya kumshukuru Mungu anayetupa uzima huu tulio nao kwa Neema, yaani bure bila kulipia chochote. hivyo basi ni maombi yangu kwa Mungu kukusaidia kuelewa somo hili ambalo ni muhimu sana kwa kanisa la sasa kuliko unavyoweza kufikiri na kuyaweka katika matendo yale utakayojifunza. Fuatana na mimi katika somo hili ili uwe sehemu ya mabadiliko ambayo Mungu anataka kuyafanya katika Kanisa ambalo ni mimi pamoja na wewe.

Unaposoma Biblia katika kitabu kile cha Matendo ya Mitume 3:19 Biblia inasema ‘…Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake…”

Katika tafsiri ya the living Bible  Biblia inasema “…Now change your mind and attitude to God and turn to Him so that He can cleanse away your sins and send you wonderful times of refreshment from the presence of the Lord…”

Unaposoma katika tafsiri hizi zote mbili za Biblia unapata maana nzuri ya TOBA ambayo ni kurejea na kuacha kufanya kitu ambacho ulikuwa unakifanya na Mungu hataki na hapendi wewe ukifanye.Biblia ya kiingeleza imesema “ Change your mind and attitude ” kwa iyo unaona kuwa TOBA ni kubadilisha mtazamo wako na mawazo kumulelekea Mungu na kuacha kuelekea dhambi. Kinachomfanya Mungu akusamehe dhambi zako ni kule kubadilisha mtazamo wako na mawazo yako yasiyoendana na Mungu. Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa TOBA ni kugeuka kutoka katika jambo ambalo Mungu amelikataza na kutenda lile ambalo Mungu ameliagiza kufanya

Si suala tu la kugeuka lakini ni kuenda mbali na yale mambo ambayo Mungu amekuambia kwa Neno lake ya kuwa usifanye

CHANZO CHA TOBA
Toba imekuja kwa sababu ya dhambi kusingekua na Toba kama hakuna dhambi na Bilbia inatuambia dhambi ni uasi (1 Yohana 3:4) na uasi ni kuenda kinyume na maagizo ya Mungu. Kwa iyo kilichosababisha dhambi ije na kutawala duniani ni uasi ambao mwanadamu aliufanya dhidi ya Mungu.
Dhambi iliingia duniani kwa njia ya KUSIKIA, KUAMINI na KUTII uongo wa shetani.Adamu ambaye ni mwanadamu wa kwanza na mtangulizi wetu kama baba yetu wa kwanza ALISIKIA, ALIAMINI, na AKATII uongo wa shetani na ivyo akaruhusu dhambi kuingia ulimwenguni. Warumi 5:12

“…Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi…”

Aliyesikia ni Adamu aliyeamini ni Adamu na aliyetii uongo wa shetani ni Adamu lakini dhambi ikatufikia watu wote kwa kuwa tu uzao wa Adamu wa kwanza. Unaposikia unapoamini na unapotii kile ambacho shetani kwa kupitia kitu chochote amekushawishi kukifanya unatenda dhambi juu ya Mungu na ndipo TOBA inahitajika katika maisha yako.Mungu hapendi wanadamu waishi chini ya mfumo wa dhambi na ndio maana alianzisha mfumo mpya kwa mwanadamu wa kumrudia yeye baada ya kukosea na mfumo huo ni kwa njia ya TOBA. Alimfanya mwanawe Yesu Kristo asiye na dhambi kuwa dhambi ili kwa kupitia yeye aliye mkamilifu wanadamu wapate ondoleoo la dhambi milele (1Korintho 5:21)

Kwa hiyo toba iliingia kwa njia ya KUSIKIA, KUAMINI na KUTII kile ambacho Mungu amesema.Yesu ambaye ni Adamu wa mwisho (1 Korintho 15:45) ALISIKIA, AKAAMINI na KUTII maagizo ya Mungu na ivyo kuuondoa ule uasi ambao Adamu wa kwanza aliufanya. hivyo kwako wewe ambaye ni sehemu ya Kanisa la Mungu unapata TOBA kwa KUSIKIA, KUAMINI na KUTII maagizo ya Mungu katika maisha yako

KWA NINI TUNAHITAJI TOBA
Kuna mambo mengi ambayo hayaendi sawa katika kanisa la Mungu na ili yaende sawa tunamuhitaji Mungu aingilie kati kwa njia ya TOBA.Kama Kanisa la Mungu nikimaanisha mtu aliye mwamini YESU KRISTO likikosea au akikosea mambo mengi katika maisha yake na ya watu wengine wanaounganishwa naye hayawezi kuenda sawa hii ikiwa na maana kuanzia katika ngazi ya chini kabisa katika familia na hata ngazi ya juu zaidi katika taifa hayawezi kuenda sawa maana kuna makosa yaliyofanywa na hayajatubiwa

Ukisoma katika kitabu kile cha Warumi 3:23 utaelewa vizuri kile ninachosema Biblia inasema “… kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;…”

Unapofanya dhambi yoyote katika maisha yako utukufu na uwepo wa Mungu katika maisha yako unapungua na hivyo kufanya kiwango cha Mungu kushugulika na maisha yako kupungua siku hadi siku. Kwa hiyo wewe kama sehemu ya kanisa unapokuwa umefanya dhambi na haujatubu UTUKUFU na UWEPO wa Mungu uliokuwa katika maisha yako unapungua na hivyo kufanya nguvu na uwepo wa Mungu uliokuwa unashugulika na maisha yako na wote wanaounganishwa na wewe kupungua katika maisha yako na unapozidi kupungua ndipo uwepo wa shetani na nguvu za shetani zinapozidi kuyatawala maisha yako na maisha ya wote uliokuwa unaunganishwa nao kama sehemu ya kanisa


Mahusiano uliyokuwa nayo na Mungu kama Kanisa yanaharibika kabisa kwa sababu ya dhambi,Mungu alikuwa rafiki yako lakini anakua adui yako huoni tena sababu ya kuwa karibu na Mungu unafanya mambo yasiyompendeza Mungu kabisa.Na hiki ndicho kilichotokea hata kwa Adamu baada ya kumuasi Mungu akaona ajifiche mbali na uso wa Mungu akijua Mungu hamuoni. Mungu anachohitaji kutoka kwako baada ya kukosea ni wewe kuomba TOBA kwake na wala sio kujificha mbali naye na kuendelea kufanya yaliyo maovu zaidi. Sio suala la kuendelea mbele kana kwamba hujui kosa ulilolifanya na hujali kwamba umefanya bali ni suala la Kurudi na kuzingatia kisha kuungama dhambi zako ulizozifanya 
Ufunuo 2:5”… Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu…” 

 Suluhisho ni kukumbuka kosa kisha kutubu na kubadilisha muelekeo uliokuwa unaenda nao.Anaposema kumbuka ni wapi ulikoanguka ukatubu hana maana kwamba uikumbuke dhambi namna ulivyofanya la hasha ana maana yakumbuke mazingira yaliyokupelekea wewe ukafanya dhambi kisha epukana na hayo mazingra na ubadilishe muelekeo wako katika mazingira yaliyokufanya umkosee Mungu. Suala la kuanguka lipo lakini Biblia inatufundisha kitu kimoja muhimu sana kuwa ukianguka USIKAE hapo hapo na kukubaliana na hali iyo bali INUKA na UTUBU. Usikae hapo hapo wala usiinuke na kuendelea mbele KANA KWAMBA hakujatokea kitu bali INUKA na UTUBU

No comments:

Post a Comment