Wednesday, September 17, 2014

WOKOVU

Inawezekana neno hili wokovu au kuokoka sio geni masikioni mwako umelisikia mara nyingi na una maana nyingi kuhusu wokovu. Lakini embu tuangalie Biblia inasemaje kuhusu wokovu

Warumi 10:9-10 Biblia inasema “… Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu…”

hivyo kwa tafsiri iliyo nyepesi WOKOVU ni kumkubali Yesu Kristo kuwa ni Bwana
Na Mwokozi wa maisha yako. Unamkubali moyoni mwako na kusema kwa kinywa chako kile ulichokiamini na kukikubali moyoni mwako.

Kwa hiyo wokovu au kuokoka ni KUAMINI moyoni na KUKIRI mdomoni ya kuwa YESU KRISTO ni Mwana wa Mungu na yakuwa Mungu alimtuma ili aje kuwaokoa wanadamu ambao ni mimi na wewe, kila anaye amini ya kwamba YESU KRISTO alitumwa na Mungu aje duniani ANAOKOKA

Yohana 3:16 “… Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele…”

Kilichomfanya Mungu amtume mwanawe tena wa pekee aje duniani kuutoa uhai wake kwa ajili ya wanadamu waliokuwa katika dhambi ni UPENDO wake juu ya wanadamu. Aliwapenda wanadamu kwanza ndipo akamtuma YESU KRISTO aje duniani kwa ajili yetu.
Kila mtu anaye mwamini YESU KRISTO anafanyika kuwa mwana wa Mungu na kuingia katika ufalme wa Mungu ulio wa milele.

Mungu hakutamani na wala hatamani kuona wanadamu wanapotea nje na Kweli yake, ndio maana Yesu Kristo alikuja ili atuonyeshe Njia itupasayo kuiendea ili tusizidi kupotea

Yohana 14:6 “…Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi…”

Mungu anataka wanadamu wote tuijue Njia yakumfikia yeye na Njia hiyo ni YESU pekee hakuna NJIA nyingine ya kumfikia Mungu isipokuwa kwa kupitia YESU KRISTO pekee, kwa sababu hiyo ukimwamini YESU KRISTO kuwa Bwana na Mwokozi na Kiongozi wa maisha yako UTAOKOKA na kuupokea uzima wa milele ndani yako na hatimaye utamfikia Mungu na kumuona Mungu na kuishi naye milele na milele
Mathayo 10:32-33
“…Basi kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni…”

Unayo nafasi sasa ya kumpa Yesu maisha yako UKIAMINI kwa moyo wako na KUKIRI kwa kinywa chako kuwa YESU KRISTO ni BWANA na Mwokozi na Jina lako litaandikwa Mbinguni; Yesu ameahidi Kukukiri Mbele za MUNGU mbinguni lakini pia kama ukimkana huku duniani kwa kutoamini naye pia atakukana mbele za Baba yake aliye mbinguni.

Ikiwa hujaokoka na ungependa kuokoka sema nami sala hii kwa sauti hapo ulipo
Nakushukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wako kwangu, nakushukuru kwa kumtuma mwanao YESU KRISTO aje kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu, naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha yangu, futa jina langu kwenye kitabu cha mauti na andika jina langu kwenye kitabu cha UZIMA, kuanzia leo mimi ni mali yako. namkataa shetani na kazi zake zote, unipe ROHO wako akae nami siku zote za maisha yangu; katika Jina la YESU KRISTO Amen.

Ikiwa umesema sala hiyo basi tayari umeokoka na Yesu Kristo yuko ndani yako kwa imani
Mungu azidi kuwa nawe akikufundisha na kukutunza katika Jina la YESU Amen.

tafuta kanisa lililo karibu nawe linaloamini na kufundisha habari za wokovu na ondoleo la dhambi za wanadamu ukajiunge nao ili uendelee kuukulia wokovu wako.

No comments:

Post a Comment