Tuesday, September 9, 2014

MAFUNDISHO

Mwl Erasto Kibiki
NAMNA YA KUFANIKIWA KATIKA ELIMU

Sehemu ya kwanza
Kila mtu ana namna na mfumo wake wa kusoma, lakini namna unavyosoma sasa inaweza kuwa haikufai zaidi katika mafanikio yako kielimu. Utajuaje? Ni rahisi tu! Kama matokeo yako katika mitihani mbalimbali hayalingani na matarajio ya ufaulu wako uliyojiwekea, basi inatakiwa ubadilishe namna unavyosoma.

Dunia ya leo ipo katika mabadiliko makubwa sana yanayotokana na kuongezeka kwa maarifa, na kuendelea kwa sayansi na teknolojia kama ilivyotabiriwa kuwa “Hata wakati wa mwisho wengi wataenda mbio huko na huko na maarifa yataongezeka” (Danieli 12:4c) hali inayopelekea elimu kuhitajika sana na kuwa na thamani zaidi ukilinganisha na kabla ya mabadiliko haya kutokea.

Katika kitabu hiki, nimeelezea kwa sehemu dhana nzima ya elimu, utofauti wake na masomo ya darasani, mambo muhimu ya kufanya ili kila mtu afanikiwe katika elimu yake na aina nyingine za elimu ambazo upatikanaji wake hutofautiana kulingana na mahitaji ya kila mtu.

TAFSIRI YA ELIMU
Elimu ni ujuzi aupatao mtu kwa njia yoyote unaomsaidia kuishi hapa duniani kwa maisha ya sasa na yajayo; ujuzi huu waweza kupatikana kwa njia ya asili au kwa njia isiyo ya asili. Elimu ni ufunguo wa ukombozi na chombo muhimu cha kupunguza matatizo ya jamii na uchumi, kwani elimu ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi.

Katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa kimaksudi na jamii kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Maana mbalimbali za elimu zina dhana kuu moja ambayo ni kupitisha maarifa katika vizazi tofauti tofauti.

Upana wa elimu huthibitisha kuwa kiwango cha maarifa hapa duniani kimeongezeka kama ilivyotabiriwa katika maandiko matakatifu kuwa “…hata wakati wa mwisho, wengi wataenda mbio huko na huko na maarifa yataongezeka”. (Daniel 12:4) zaidi ya yote “ Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike maana yeye ni uzima wako” (Mithali 4:13).

Ujuzi wowote ulionao ndiyo elimu yenyewe, hivyo Maisha bila elimu ni sawa na bure, ndio maana tunatakiwa kuwa na ujuzi wowote  utakaotusaidia kuishi vizuri hapa duniani, hapa mtunzi wa mithali hii ameifananisha elimu na kiumbe hai, hata akasema “mshike maana yeye ni uzima wako” hivyo kiwango cha maisha utakayoishi hapa duniani kinategemeana na aina ya ujuzi ulionao na jinsi unavyoutumia.

Mafanikio ya kielimu yana gharama zake zinazotakiwa kulipwa na mhusika kwa wakati na majira sahihi, uwe na uhakika kuwa ujuzi huu utakusaidia sana katika shule yako na maisha kwa ujumla.

AINA ZA ELIMU
Kwa kawaida elimu ni pana sana, kama tunavyojua kuwa ujuzi wowote alionao mtu huitwa elimu kama elimu ya biashara, elimu ya ufundi, elimu ya viumbe hai, elimu ya maisha na kadharika. Elimu hufananishwa na ghara lililojaa aina mbalimbali za vyakula na kama mafuta ghafi ambayo yakichujwa hutoa aina mbalimbali za mafuta kama Diesel, Petrol na mafuta ya taa.

Masomo ya darasani ni sehemu ya elimu na wala sio elimu yenyewe, ni kama kitendea kazi ndani ya elimu na zipo aina kuu mbili za elimu ambazo ni Elimu rasmi na Elimu isiyo rasmi na ndani yake kuna aina ndogo ndogo za elimu zinazounda aina kuu mbili za elimu kama zilivyotajwa hapo juu.

1.      ELIMU RASMI - [ formal education]
Hii ni aina ya elimu tunayoipata darasani moja kwa moja kwa kutumia masomo maalum yanayofundishwa na walimu wetu, kwa kawaida aina hii ya elimu imewekwa na kupangwa kwa madaraja mbalimbali kuanzia ngazi ya shule ya msingi mpaka chuo kikuu; madaraja makuu ni elimu ya msingi, elimu ya sekondari na elimu ya juu {chuo kikuu}.

Pia inahusisha masomo ya taaruma kwa ujumla na aina mbalimbali za mipango {program} maalum kwa wanafunzi wanaosoma muda wote {full time students}, kwa wale wanaosomea elimu ya ufundi na utaalam ambao hupelekea kutunukiwa vyeti. Elimu hii hufuata mtaala maalum unaoisha kwa kipindi maalum wenye himizo maalum katika mitihani na kutunukiwa vyeti.

Jamii huitambua sana elimu hii na mtu ambaye hajaenda shule hudharauliwa na kuonekana kama hajaelimika hata kama ana ujuzi unaomfanya aishi vizuri kitu ambacho si kweli.

NGAZI ZA ELIMU RASMI
Elimu rasmi ina ngazi kuu mbili ambazo ni elimu ya kawaida na elimu ya juu. Elimu ya kawaida ina vipengere vifuatavyo. Elimu ya msingi, Elimu ya sekondari (O-LEVEL & A-LEVEL), ngazi ya cheti (Certificate) na ngazi ya Diploma. Kwa kawaida mtu anayefauru katika ngazi hizi hupata fursa ya kusoma elimu ya juu.

Elimu ya juu ina ngazi zifuatazo, ngazi ya shahada ya kwanza (Degree), ngazi ya uzamili –shahada ya pili (Masters), ngazi ya uzamivu au shahada ya tatu (Doctorate) na hatimaye kuwa mtaalam maalum yaani uprofesa (Profession).

2.      ELIMU ISIYO RASMI (Informal education)

Huu ni mchakato wa kuyapata maarifa au ujuzi na mbinu mbalimbali kutokana na mitazamo tofauti tofauti inayopatikana siku hadi siku pale ambapo mtu anashabiliana na mazingira yanayomzunguka.

Mchakato huu hauna mpangilio maalum, wala mwongozo rasmi na haujawa na lengo maalum; watu huipata elimu hii kwa kuchunguza mambo na kuhusika moja kwa moja pale wanapohusishwa kufanya kazi au jambo Fulani la kijamii katika mfumo wa maisha ya kila siku. Kwa kupitia mshabiliano (interaction) ndani ya familia, wakati wa matembezi, safarini, masokoni, maktaba, kwa njia ya vyombo vya habari na maeneo yoyote yenye watu.

Ndani ya tamaduni mbalimbali zisizojua kusoma wala kuandika, elimu hii huchukua sehemu kubwa sana ya kuelimisha jamii na kuendeleza maarifa kwa kizazi kimoja na kingine. Hivyo umuhimu wa elimu hii ni katika kumwezesha mtu kukabiliana na changamoto za mara kwa mara na kukidhi mahitaji yake. Na elimu za aina zote ni muhimu kwani hutegemeana na zote hupitisha maarifa kizazi hadi kizazi.

UMUHIMU WA KUWA NA BIDII KATIKA ELIMU

Bidii inahitajika katika kufanikisha jambo lolote, na kujibidiisha katika kuipata elimu hutoa nafasi kubwa ya kufikia viwango vikubwa vya mafanikio maishani, ni vyema sana kufanya kazi kwa bidii ili ule chakula chako mwenyewe na unywe maji ya birika lako mwenyewe.

Zaidi sana “Yafahamu sana haya nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote” (2Timotheo 2:7) hii ikiwa ni pamoja na masomo ya darasani. Kwa wanafunzi walioko sekondari ambao ni O-level na A-level, ni muhimu kusoma sana ili kufikia kiwango cha elimu ya juu (Chuo kikuu) ambayo huongeza kwa kiasi kikubwa sana cha kufikiri na kutatua matatizo yanayotukabiri.

Kwa waliopo vyuoni, GPA nzuri ni ya muhimu kazini na katika maisha kwa ujumla hasa aina ya ujuzi unaoupata yafaa sana ukawa tayari kuupata kwa bidii na nguvu zako zote. Si vyema kukata tama mapema katika kutafuta mafanikio kielimu kwani “hata wao walianza kama sisi” nasi tunayaweza mambo yote katika Yeye atutiaye nguvu.

Uvivu ni kizuizi kikuu cha mafanikio ya elimu kwa mwanafunzi, hata Mungu hapendi watu wavivu na “Ikiwa mtu hataki kufanya kazi (kusoma), basi na asile chakula (asifauru mitihani yake)” [1 Thesalonike 3:10] naam apandacho mtu ndicho avunacho.

Kwa mantiki hiyo, kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mwanafunzi yeyote hutegemea sana namna ya kujipanga na kukabiliana na changamoto zilizoko katika elimu. Si rahisi sana kufikia viwango vya juu vya kupata elimu rasmi (formal education) kama hazijalipwa gharama za kutosha katika upatikanaji wa elimu.

TOFAUTI ILIYOPO KATI YA ELIMU NA MASOMO YA DARASANI
Kama ilivyoelezwa hapo awali kuwa Elimu ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi uzoefu huu unaopatikana kwa njia mbalimbali na kwa gharama kubwa huifadhiwa katika akili ya mwanadamu kwa kipindi kirefu hasa ukizingatia kuwa thamani ya elimu iko juu sana nyakati hizi ukulinganisha na  vitu vingine.

Masomo hasa yale ya darasani ni mfumo uliochaguliwa kuelezea aina furani ya elimu ili kurahisisha upatikanaji wake. Masomo ni sehemu tu ya elimu na wala sio elimu yenyewe, kwa mfano; Elimu ya viumbe hai inaelezewa kwa somo la biolojia wakati Elimu ya mambo ya kale huelezewa kwa somo la Historia n.k

Ni muhimu kama msomi mtarajiwa wa kizazi hiki na kijacho kuwa makini sana na aina ya elimu unayoitaka maishani, kwani elimu ni uzima wako wa sasa na wa baadae kwa kutegemeana na aina ya ujuzi na namna ulivyopatikana huo ujuzi. Akili ambazo Mungu amemkirimia kila mtu ni za hadhi ya juu sana na zipo ili kutufikisha mahali tunatakiwa kufika.

Hata hivyo maisha ni zaidi ya kufauru masomo ya darasani kwani ujuzi wa kilimo, biashara, mazingira na aina nyingine za elimu humwezesha mtu kufanikiwa kimaisha.


Jifunze nasi, itaendelea………………………………….

No comments:

Post a Comment