Thursday, September 25, 2014

VITA DHIDI YA HATIMA YA MAISHA YAKO

Mwl. ERASTO KIBIKI
Hatima ni lile kusudi la milele ambalo mwanadamu ameumbiwa alitimize akiwa hapa duniani, kama tunavyosoma katika biblia kuwa “Daudi baada ya kulitimiza kusudi la Mungu wake akalala na baba zake

Hatima {Destiny}  ni ule wito unaokufanya uishi hapa duniani na baada ya kuukamilisha unarudi mbinguni kwa Mungu wako.

Hatima ya maisha ni kitu muhimu sana kukijua kabla ya kuvijua vitu vyote, maana hatima ni zile ndoto za maisha yako ambazo kwa hizo unakula, unakunywa, unapata makazi na malazi. Kwa hatima yako unapata pesa inayokuwezesha kuishi vizuri na kuwa msaada katika jamii inayokuzunguka.
Wengi wamekufa wangali bado wanahitajika hapa duniani, wamezikwa na ndoto zao zisizotimizika, wamepoteza heshima zao na maisha yao yaliyokuwa tegemeo kubwa sana duniani kote, kilio chao kinasikika masikioni mwa wengi, wanajiuliza sana kwa nini watu wema wanakufa mapema kuliko watu wabaya, maana wabaya wanaishi miaka mingi wakiendelea kutenda uovu.

Si hivyo hii ni vita ya hatima za maisha ya watu, ni mkakati wa shetani na malaika zake wa kuwafanya watu wasiwe msaada kwa jamii zao, kuwabadilishia hatima za maisha ili waishi maisha feki, maana maisha yako ya asili ambayo Mungu amekuumbia uyaishi yametekwa nyara na ndoto zako za maisha zimeibiwa na kufichwa kwenye mapango na mashimo ya kichawi.
Wewe ulikusudiwa kabisa uwe meneja au mmiliki wa kampuni yako, uliumbiwa kuwa mwanasheria kabisa ili haki itendeke, uwe mwalimu ili vijana wapate elimu bora na Mungu atukuzwe kupitia wewe, lakini umejikuta unaishia kuwa mama ntilie, au mbeba mizigo wa stendi, au mtu anayeishi maisha yaliyo chini ya kiwango. Hapo hatima yako imetekwa, imeibiwa na adui amekushinda vitani. Hiyo ni vita lazima upambane kuikomboa kesho yako.
Wengi wanapokutana na magumu ya kimaisha, na mambo mabaya maishani wanatiana moyo wakisema kuwa “usilie! Jikaze kiume! Maana maisha ndivyo yalivyo, vumilia!” bila kuchunguza kwa undani chanzo cha tatizo, hatimaye wanaangukia katika mtego wa ibilisi na kuangamia.

Si kila ugumu wa maisha ndivyo ulivyo au ndivyo unavyotakiwa kuwa! Hapana! Kila kitu kina chanzo chake, inuka ukaishindanie hatima yako, huo ni uonezi na ni mbinu chafu za adui za kukuibia Baraka zako. Uwe hodari na jasiri katika Bwana maana hii ni vita kamili inayopiganwa katika ulimwengu wa roho, jikaze kiume maana bila shaka utashinda, Mungu yuko upande wako; tena walio upande wetu ni wengi kuliko walio katika upande wa adui.

Hatima ya maisha yako [your Destiny] ni mahali ulipokusudiwa ufike na uishi hapo ili ulitumikie na kulitimiza shauri/kusudi la muumba wako uliloletwa kwalo na ndilo linalokufanya uishi, ukiisha kulitumikia shauri hilo hakika yake utalala na baba zako kaburi, yaani kifo kitakupata nawe hutaonekana tena juu ya uso wa nchi bali utaenda kuishi milele mbinguni au jehanamu kwa kutegemeana na uhusiano wako na Mungu wako ulipokuwa hai.
Maisha haya ya kulitumikia na kulitimiza kusudi uliloumbwa nalo yamefichwa ndani ya muda na nyakati maalum chini ya mbingu, maana “kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa; wakati wa kupanda na wakati wa kung’oa yaliyopandwa. …… Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo?” [Mhubiri 3:1-9] ni muhimu sana kuzijua nyakati na majira ya maisha yako. Je! Hapo ulipo ndipo kusudi lako la kiuumbaji lilipo? Je! Ndipo wito wako ulipo? Na je! Huo wito unautimiza ndani ya muda maalum.
Maana hata Gideon aliitwa kwa wakati na majira yake ili awaokoe waisraeli dhidi ya mateso ya wamidian, na alipotendwa kwa wakati uliokusudiwa Mungu alimhesabia haki, malkia Esta hakulitambua kusudi la uwepo wake duniani, yaani hakujua hatima ya maisha yake mpaka pale ndugu yake Mordekai alipomwambia “… kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea wayahudi msaada wa wokovu kwa njia nyingine, ila wewe utaangamia pamoja na mlango wa baba yako. Walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?” [Esta 4:12-17]
Eti! Ndugu yangu ni nani ajuaye kama elimu na hadhi uliyonayo ni ili uwaletee ndugu zako ukombozi dhidi ya umaskini, ugumu wa maisha na hali tete ya familia na jamii yako? Yumkini umekuwa kiongozi ili ulijenge taifa lako katika hali ya kumcha Mungu na kuimarisha maisha ya watu wako wengi waliokata tamaa ya kuishi. Ni nani ajuaye kama uzuri ulionao ni kwa ajili ya ufalme wa Mungu na si ukahaba unaoufanya! Ni nani ajuaye kama hatima yako ipo ili hali njema ya maisha ya watu itokee nawe uwe Baraka kwao.
Adui anafanya vita dhidi yako ili kuziua ndoto za maisha yako, hakutafuti wewe bali anaitafuta hatima ya maisha yako popote ulipo. Ndipo sasa unapaswa kujua namna ya kuishindania hatima yako, umezaliwa ili uwe mshindi siku zote, wewe ni zaidi ya vile ulivyo, usujidharau kwa vyovyote, umepewa uwezo na mamlaka ipo ndani yako. Kabisa unapaswa kujua aliye ndani yako ni mkuu kuliko wale wanaokutafuta maishani.
AINA KUU MBILI ZA MAADUI WA HATIMA YAKO
Wapo maadui wakuu wawili wa hatima ya maisha yako, wanakuwinda usiku na mchana ili kukuangusha na kukupoteza katika uso wa nchi, maadui hawa kwa asili ni mapacha na wamegawana majukumu ili kukushambulia ipasavyo nao ni
1.     Adui wa ndani
2.     Adui wa nje
Kiasili hivi ni vyeo tu, yaani kila aina ya adui ndani yake kuna idara na uongozi mbalimbali unaotenda kazi katika ulimwengu wa roho. Ni sharti kuwafahamu vizuri na kuzijua mbinu za kuwashinda na kuwa mshindi kweli kweli.
Adui mbaya zaidi ni Yule wa ndani yako, yeye anaishi na anatenda kazi kutokea ndani yako, katika fikra na akili zako, katika moyo wako, katika viungo vyako vya mwili n.k
Adui wa nje anategemea sana msaada kutokea ndani, yeye amepewa jukumu la kumsadia adui wa ndani na kumuongezea nguvu za kiutendaji kazi tu.

No comments:

Post a Comment