 |
Mwl Erasto Kibiki |
NAMNA YA KUFANIKIWA KATIKA ELIMU
Sehemu ya kwanza
Kila mtu ana namna na mfumo wake wa kusoma, lakini namna
unavyosoma sasa inaweza kuwa haikufai zaidi katika mafanikio yako kielimu.
Utajuaje? Ni rahisi tu! Kama matokeo yako katika mitihani mbalimbali
hayalingani na matarajio ya ufaulu wako uliyojiwekea, basi inatakiwa ubadilishe
namna unavyosoma.
Dunia ya leo ipo katika mabadiliko makubwa sana yanayotokana
na kuongezeka kwa maarifa, na kuendelea kwa sayansi na teknolojia kama
ilivyotabiriwa kuwa “Hata wakati wa mwisho wengi wataenda mbio
huko na huko na maarifa yataongezeka” (Danieli 12:4c) hali inayopelekea
elimu kuhitajika sana na kuwa na thamani zaidi ukilinganisha na kabla ya
mabadiliko haya kutokea.
Katika kitabu hiki, nimeelezea kwa sehemu dhana nzima ya
elimu, utofauti wake na masomo ya darasani, mambo muhimu ya kufanya ili kila
mtu afanikiwe katika elimu yake na aina nyingine za elimu ambazo upatikanaji
wake hutofautiana kulingana na mahitaji ya kila mtu.
TAFSIRI YA ELIMU
Elimu ni ujuzi aupatao mtu kwa njia yoyote unaomsaidia kuishi
hapa duniani kwa maisha ya sasa na yajayo; ujuzi huu waweza kupatikana kwa njia
ya asili au kwa njia isiyo ya asili. Elimu ni ufunguo wa ukombozi na chombo muhimu
cha kupunguza matatizo ya jamii na uchumi, kwani elimu ni tendo au uzoefu wenye
athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi.
Katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa
kimaksudi na jamii kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kizazi kimoja
hadi kingine. Maana mbalimbali za elimu zina dhana kuu moja ambayo ni kupitisha
maarifa katika vizazi tofauti tofauti.
Upana wa elimu huthibitisha kuwa kiwango cha maarifa hapa
duniani kimeongezeka kama ilivyotabiriwa katika maandiko matakatifu kuwa “…hata
wakati wa mwisho, wengi wataenda mbio huko na huko na maarifa yataongezeka”.
(Daniel 12:4) zaidi ya yote “ Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike
maana yeye ni uzima wako” (Mithali 4:13).
Ujuzi wowote ulionao ndiyo elimu yenyewe, hivyo Maisha bila
elimu ni sawa na bure, ndio maana tunatakiwa kuwa na ujuzi wowote utakaotusaidia kuishi vizuri hapa duniani,
hapa mtunzi wa mithali hii ameifananisha elimu na kiumbe hai, hata akasema “mshike maana yeye ni uzima wako” hivyo
kiwango cha maisha utakayoishi hapa duniani kinategemeana na aina ya ujuzi
ulionao na jinsi unavyoutumia.
Mafanikio ya kielimu yana gharama zake zinazotakiwa kulipwa
na mhusika kwa wakati na majira sahihi, uwe na uhakika kuwa ujuzi huu utakusaidia
sana katika shule yako na maisha kwa ujumla.
AINA ZA ELIMU
Kwa kawaida elimu ni pana sana, kama tunavyojua kuwa ujuzi
wowote alionao mtu huitwa elimu kama elimu ya biashara, elimu ya ufundi, elimu
ya viumbe hai, elimu ya maisha na kadharika. Elimu hufananishwa na ghara
lililojaa aina mbalimbali za vyakula na kama mafuta ghafi ambayo yakichujwa
hutoa aina mbalimbali za mafuta kama Diesel, Petrol na mafuta ya taa.
Masomo ya darasani ni sehemu ya elimu na wala sio elimu
yenyewe, ni kama kitendea kazi ndani ya elimu na zipo aina kuu mbili za elimu
ambazo ni Elimu rasmi na Elimu isiyo rasmi na ndani yake kuna aina ndogo ndogo
za elimu zinazounda aina kuu mbili za elimu kama zilivyotajwa hapo juu.
1. ELIMU RASMI - [ formal education]
Hii ni aina ya elimu tunayoipata darasani moja kwa moja kwa
kutumia masomo maalum yanayofundishwa na walimu wetu, kwa kawaida aina hii ya
elimu imewekwa na kupangwa kwa madaraja mbalimbali kuanzia ngazi ya shule ya
msingi mpaka chuo kikuu; madaraja makuu ni elimu ya msingi, elimu ya sekondari
na elimu ya juu {chuo kikuu}.
Pia inahusisha masomo ya taaruma kwa ujumla na aina
mbalimbali za mipango {program} maalum kwa wanafunzi wanaosoma muda wote {full
time students}, kwa wale wanaosomea elimu ya ufundi na utaalam ambao hupelekea
kutunukiwa vyeti. Elimu hii hufuata mtaala maalum unaoisha kwa kipindi maalum
wenye himizo maalum katika mitihani na kutunukiwa vyeti.
Jamii huitambua sana elimu hii na mtu ambaye hajaenda shule
hudharauliwa na kuonekana kama hajaelimika hata kama ana ujuzi unaomfanya aishi
vizuri kitu ambacho si kweli.
NGAZI ZA ELIMU RASMI
Elimu rasmi ina ngazi kuu mbili ambazo ni elimu ya kawaida na
elimu ya juu. Elimu ya kawaida ina vipengere vifuatavyo. Elimu ya msingi, Elimu
ya sekondari (O-LEVEL & A-LEVEL), ngazi ya cheti (Certificate) na ngazi ya
Diploma. Kwa kawaida mtu anayefauru katika ngazi hizi hupata fursa ya kusoma
elimu ya juu.
Elimu ya juu ina ngazi zifuatazo, ngazi ya shahada ya kwanza
(Degree), ngazi ya uzamili –shahada ya pili (Masters), ngazi ya uzamivu au
shahada ya tatu (Doctorate) na hatimaye kuwa mtaalam maalum yaani uprofesa
(Profession).
2. ELIMU ISIYO RASMI (Informal education)
Huu ni mchakato wa kuyapata maarifa au ujuzi na mbinu
mbalimbali kutokana na mitazamo tofauti tofauti inayopatikana siku hadi siku
pale ambapo mtu anashabiliana na mazingira yanayomzunguka.
Mchakato huu hauna mpangilio maalum, wala mwongozo rasmi na
haujawa na lengo maalum; watu huipata elimu hii kwa kuchunguza mambo na
kuhusika moja kwa moja pale wanapohusishwa kufanya kazi au jambo Fulani la
kijamii katika mfumo wa maisha ya kila siku. Kwa kupitia mshabiliano
(interaction) ndani ya familia, wakati wa matembezi, safarini, masokoni,
maktaba, kwa njia ya vyombo vya habari na maeneo yoyote yenye watu.
Ndani ya tamaduni mbalimbali zisizojua kusoma wala kuandika,
elimu hii huchukua sehemu kubwa sana ya kuelimisha jamii na kuendeleza maarifa
kwa kizazi kimoja na kingine. Hivyo umuhimu wa elimu hii ni katika kumwezesha
mtu kukabiliana na changamoto za mara kwa mara na kukidhi mahitaji yake. Na elimu
za aina zote ni muhimu kwani hutegemeana na zote hupitisha maarifa kizazi hadi
kizazi.
UMUHIMU WA KUWA NA
BIDII KATIKA ELIMU
Bidii inahitajika katika kufanikisha jambo lolote, na
kujibidiisha katika kuipata elimu hutoa nafasi kubwa ya kufikia viwango vikubwa
vya mafanikio maishani, ni vyema sana kufanya kazi kwa bidii ili ule chakula
chako mwenyewe na unywe maji ya birika lako mwenyewe.
Zaidi sana “Yafahamu sana haya nisemayo, kwa maana Bwana
atakupa akili katika mambo yote” (2Timotheo 2:7) hii ikiwa ni pamoja na masomo
ya darasani. Kwa wanafunzi walioko sekondari ambao ni O-level na A-level, ni
muhimu kusoma sana ili kufikia kiwango cha elimu ya juu (Chuo kikuu) ambayo
huongeza kwa kiasi kikubwa sana cha kufikiri na kutatua matatizo
yanayotukabiri.
Kwa waliopo vyuoni, GPA nzuri ni ya muhimu kazini na katika
maisha kwa ujumla hasa aina ya ujuzi unaoupata yafaa sana ukawa tayari kuupata
kwa bidii na nguvu zako zote. Si vyema kukata tama mapema katika kutafuta
mafanikio kielimu kwani “hata wao walianza kama sisi” nasi tunayaweza mambo
yote katika Yeye atutiaye nguvu.
Uvivu ni kizuizi kikuu cha mafanikio ya elimu kwa mwanafunzi,
hata Mungu hapendi watu wavivu na “Ikiwa
mtu hataki kufanya kazi (kusoma), basi na asile chakula (asifauru mitihani
yake)” [1 Thesalonike 3:10] naam apandacho mtu ndicho avunacho.
Kwa mantiki hiyo, kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mwanafunzi
yeyote hutegemea sana namna ya kujipanga na kukabiliana na changamoto zilizoko
katika elimu. Si rahisi sana kufikia viwango vya juu vya kupata elimu rasmi
(formal education) kama hazijalipwa gharama za kutosha katika upatikanaji wa
elimu.
TOFAUTI ILIYOPO KATI
YA ELIMU NA MASOMO YA DARASANI
Kama ilivyoelezwa hapo awali kuwa Elimu ni tendo au uzoefu wenye
athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi uzoefu
huu unaopatikana kwa njia mbalimbali na kwa gharama kubwa huifadhiwa katika
akili ya mwanadamu kwa kipindi kirefu hasa ukizingatia kuwa thamani ya elimu iko
juu sana nyakati hizi ukulinganisha na
vitu vingine.
Masomo hasa yale ya darasani ni mfumo uliochaguliwa kuelezea
aina furani ya elimu ili kurahisisha upatikanaji wake. Masomo ni sehemu tu ya
elimu na wala sio elimu yenyewe, kwa mfano; Elimu ya viumbe hai inaelezewa kwa
somo la biolojia wakati Elimu ya mambo ya kale huelezewa kwa somo la Historia
n.k
Ni muhimu kama msomi mtarajiwa wa kizazi hiki na kijacho kuwa
makini sana na aina ya elimu unayoitaka maishani, kwani elimu ni uzima wako wa
sasa na wa baadae kwa kutegemeana na aina ya ujuzi na namna ulivyopatikana huo
ujuzi. Akili ambazo Mungu amemkirimia kila mtu ni za hadhi ya juu sana na zipo
ili kutufikisha mahali tunatakiwa kufika.
Hata hivyo maisha ni zaidi ya kufauru masomo ya darasani
kwani ujuzi wa kilimo, biashara, mazingira na aina nyingine za elimu humwezesha
mtu kufanikiwa kimaisha.
Jifunze nasi, itaendelea………………………………….